Wasichana waliobobea katika teknolojia Kenya

Je, unataka programu ya kulipia nauli kwenye gari, ama, programu ya kutafuta viungo vya mwili kwenye simu yako? Wasichana nchini Kenya wanatengeneza programu hizo, chini ya uongozi wa shirika la kimataifa linalowapa wasichana elimu ya kutengeneza programu za simu.
Harriet Karanja, 16, alikuwa kwenye foleni akisubiri kununua tiketi ya kusafiri kwa basi jijini Nairobi, wakati mama mmoja aliyekuwa kwenye foleni alipokonywa mali yake na wezi.
Aliposimulia tukio hilo kwa wenzake wanne shuleni, aligundua kwamba pia wao walikuwa wameshuhudia tatizo sawa na hilo.
"Itakuwaje iwapo tutabuni njia ya kuwaondoa watu kwenye foleni kununua tiketi?" Harriet akauliza.
Baadaye waliamua kutengeneza programu ya simu (App) ya kurahisisha ununuzi wa tiketi za usafiri, kwa magari ya masafa marefu.
"Programu hii inakuongoza hadi kwenye kituo cha basi kwa kutumia teknolojia ya kugundua maeneo (GPS). Badala ya kwenda kupanga foleni, utaenda tu kuabiri."
Wameipa jina 'M- Safiri'
Mashindano ya teknolojia
Wasichana hao, wanaojitambulisha kama 'Sniper', walipata nafasi ya kwenda hadi hadi San Fransisco, Marekani kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya teknolojia kwa kutumia uvumbuzi wao, ambapo waliibuka wa pili.
Washindi walikuwa wasichana kutoka Mexico waliotengeneza programu ya kuwahimiza watu kujitolea katika kazi za jamii.

Mpango wao sasa ni kuanzisha kampuni yao ya teknolojia baada ya masomo ya shule ya upili, na pia wanapanga kuisajili programu yao na kuiweka kwenye soko la programu za simu.
Hata hivyo, hawakufaulu peke yao, walihitaji washauri, ambao waliupata pamoja na ufadhili kutoka kwa kampuni ya mawasiliano nchini Kenya Safaricom.
Priscilla Wambui anasema walinufaika sana na usaidizi huo.
"Hatukuwa tunajua jinsi ya kutengeneza programu hizo, kuandika mpango wa biashara ama kuandaa na kuwasilisha wazo la kibiashara, hayo yote huchukua muda na tulitatizika sana."
Programu ya viungo vya mwili
Si hao pekee walionufaika na mawaidha ya washauri.

Damaris Muteti, mwalimu wa shule ya upili ya wasichana ya Embakasi, Nairobi, tayari alikuwa amepata mafunzo ya kutenegeneza programu za kompyuta na simu (coding) kwa ufadhili wa kampuni ya teknolojia, Intel.
Alikumbatia wazo la mwanafunzi wake la kuunda programu ya kuunganisha wagonjwa wanaohitaji viungo vya mwili, hospitali na watu wanaotaka kutoa viungo vyao.
"Lilikuwa wazo zuri na nikaona nikisaidia msichana, atasaidia wasichana wengine, na hilo litasaidia wasichana na wanawake wengi sio Kenya pekee bali pia barani Afrika."
Wazo la Caroline Wambui, 17, mwanafunzi wa kidato cha nne, lilitokana na msiba.
"Mjombangu aliaga dunia kwa kukosa figo. Ilibidi hata tutafute figo kwenye soko haramu bila mafanikio! Ulikuwa msiba mkubwa kwetu, na singetaka mtu mwingine apitie uchungu tuliopitia."
Programu hiyo inakuwezesha kujua iwapo unaweza kutoa kiungo cha mwili kumsaidia mtu mwingine, na kujua pia mahitaji ya kimatibabu ya mgonjwa anayehitaji kiungo fulani.
Wawili hao walitengeneza programu hiyo na wamepata washirika.

Wanawake wameachwa nyuma kimtandao barani Afrika
Hata hivyo hawana uwezo wa kuitoa programu hiyo kwa umma kwa wakati huu, kwani wanasubiri mswada wa kuwawezesha watu kutoa viungo vyao vya mwili wanapoaga dunia, upitishwe kuwa sheria.
Kwa sasa, magenge ya watu wanaouza viungo vya mwili kwenye soko haramu yanapata faida kubwa kupindukia, ambapo walio na tamaa ya pesa hufanyiwa upasuaji katika hospitali ambazo hazijaidhinishwa.
Iwapo sheria hiyo itaidhinishwa, basi Wambui ataleta mabadiliko makubwa katika kuhakikisha wasichana wengine kama yeye hawapotezi jamaa zao katika njia zinazoweza kuepukika.
Hata hivyo, hadithi yake ni nadra sana barani Afrika.
Kulingana na utafiti wa wakfu wa World Wide Web, ni 20% pekee ya wanawake katika vitongoji duni katika mji mkuu wa Nairobi, sawa na mtaa anamoishi Wambui wa Mukuru kwa Njenga, wanaopata huduma za mitandao.
Ushauri, na kupata wanawake wa kuiga katika nyanja ya teknolojia, ndio njia zinazopendekezwa za kubadilisha hali ilivyo sasa, kulingana na Sylvia Mukasa, msimamizi wa shirika la Women in Tech Africa nchini Kenya.

Hakuna maoni